Arusha
Home » » SERIKALI YATUMIA BILIONI 514 KUMALIZA TATIZO LA MAJI JIJINI ARUSHA

SERIKALI YATUMIA BILIONI 514 KUMALIZA TATIZO LA MAJI JIJINI ARUSHA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (AUWSA), Mhandisi Ruth Koya wakipeana mikono na Mkandarasi-Kampuni ya Jiangxi Geo-Engineering ya China, Chen Xianghua mara baada ya kusaini mkataba wa utekelezaji wa mradi wa kuboresha huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kwa Jiji la Arusha.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (AUWSA), Mhandisi Ruth Koya akisaini mkataba wa utekelezaji wa mradi wa kuboresha huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kwa Jiji la Arusha, kushoto ni Mkandarasi kutoka Kampuni ya Jiangxi Geo-Engineering ya China, Chen Xianghua wanaotekeleza mradi huo.
Sehemu ya wageni waliohudhuria hafla ya kusaini mkataba wa utekelezaji wa mradi wa kuboresha huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kwa Jiji la Arusha.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (AUWSA), Mhandisi Ruth Koya (kushoto), Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Arusha ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Gabriel Daqarro (katikati) na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe katika hafla ya kusaini wa mkataba wa utekelezaji wa mradi wa kuboresha huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kwa Jiji la Arusha.Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe akizungumza katika hafla ya kusaini wa mkataba wa utekelezaji wa mradi wa kuboresha huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kwa Jiji la Arusha.


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa kushirikiana na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Arusha (AUWSA), leo imeingia mikataba ya Dola za Marekani 233,915,581 ambazo ni takribani Shilingi 514,614,278,200 za Tanzania kumaliza kabisa tatizo la maji katika Jiji la Arusha na Wilaya ya Hai, Mkoani Kilimanjaro.

Fedha hizo ni mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ambao wamechangia Dola za Marekani 210,962,581 na Serikali ya Tanzania ikichangia Dola 22,953,000 ili kukamilisha mradi huo.

Kazi zitakazotekelezwa ni uchimbaji wa visima virefu, ujenzi wa matenki, ulazaji wa mabomba ya majisafi na majitaka, ujenzi wa mtambo wa kutibu maji, ujenzi wa mabwawa mapya ya kutibu majitaka, ujenzi wa Makao Makuu ya Mamlaka na Ofisi za Kanda pamoja na ununuzi wa vitendea kazi.

Kukamilika kwa mradi huu kutawezesha upatikanaji wa huduma ya majisafi na salama kwa wakazi wa Jiji la Arusha kwa asilimia 100 hadi mwaka 2030 na kutapunguza kiasi cha maji yanayopotea kutoka asilimia 45 ya sasa mpaka kufikia asilimia 20. Aidha, mradi utaongeza mtandao wa kuondoa majitaka kwa asilimia 30. Mradi huu unategemea kuchochea ukuaji wa uchumi wa viwanda na kuboresha huduma nyingine za kijamii zikiwemo Afya na Elimu.

Hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Jijij la Arusha kwa sasa ni asilimia 44, sawa na wastani wa lita milioni 40 kwa siku na mradi huu unategemea kuongeza kiwango na kufikia lita milioni 200 kwa siku.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa