Arusha
Home » » CCM YATAMBA UCHAGUZI MARUDIO UDIWANI, CHADEMA WAJITOA

CCM YATAMBA UCHAGUZI MARUDIO UDIWANI, CHADEMA WAJITOA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 Imeandikwa na Waandishi Wetu
KATA 43 za Tanzania Bara katika halmashauri 36 mikoa 19, jana zilifanya Uchaguzi Mdogo wa Udiwani ulioenda vizuri sehemu mbalimbali nchini huku matokeo ya awali yakionesha wakati tukienda mitamboni kuwa wagombea wa chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM) walikuwa wamefanya vizuri katika kata mbalimbali walizosimama mkoani Arusha.
Wakati CCM kikitamba Arusha, wapinzani wao wakuu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kilitangaza kujitoa kwenye uchaguzi huo katika kata tano zilizopo wilayani Arumeru mkoani Arusha jana alasiri wakati tayari upigaji kura ukiwa unaendelea katika kata hizo. Kata walizojitoa ni Maroroni, Makiba, Ngabobo, Leguruki na Ambureni.
Wakati Chadema ikitangaza kujitoa kwa madai ya kuwapo kwa fujo, Mkurugenzi wa Uchaguzi katika Tume ya Uchaguzi (NEC), Ramadhani Kailima alieleza kuwa uchaguzi huo kwa kata zote 43 umekwenda vizuri kwa asilimia 100.
“Vituo vyote kufikia saa 10.30 jioni hali ilikuwa nzuri na kura zilikuwa zinahesabiwa. Kumekuwapo na kasoro ndogo, kwa mfano kule Mwanza kuna vijana wa Chadema walikuwa wakiwazuia watu kwenda kupiga kura Nyakato. “Dar es Salaam kila kitu kimekwenda vizuri, Lushoto kulikuwa na mawakala walitaka waruhusiwe bila kuwa na kiapo cha uwakala, lakini wakazuiwa,” alisema Kailima.
Kuhusu Chadema kujitoa, alisema suala hilo limefanyika kati ya saa 8 na 9, wakati mambo mengine yakiwa yamefanyika, na kuongeza kuwa ni haki yao, lakini suala la kurudiwa uchaguzi halipo. “Uchaguzi kwa mujibu wa sheria na kanuni unaweza kurudiwa endapo msimamizi msaidizi wa uchaguzi ataona kuna vurugu kubwa na hivyo kuchukua hatua za kuiarifu Tume.
Lakini kwa Arusha, hakuna vurugu zozote kubwa zilizotolewa na msimamizi msaidizi,” alieleza Kailima. Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, wamechukua uamuzi huo baada ya kuona rafu mbalimbali zikifanyika ikiwemo baadhi ya wabunge na viongozi mbalimbali kukamatwa na kuumizwa sehemu mbalimbali za miili yao.
Alisema wamevumilia kwa muda mrefu huku wakitegemea wenye mamlaka watatumia busara zao kusimamia utengamano na amani katika jimbo hilo, lakini wameona ni heri wajitoe tu. “Huu si uchaguzi, ni fujo Arumeru hakuna uchaguzi, watu wanapigwa na vyombo vya dola vinaangalia tu wala havichukui hatua sasa nasema wananchi wakiona wanaonewa huko walipo watafute utaratibu wao kujihami na vipigo,” Mbowe aliwaambia waandishi wa habari.
Alisema wataendelea kushiriki kwenye kata nyingine 38 zilizobakia. Wagombea waliotangaza kujitoa ni Dominick Mollel (Ambuleni), Fabiel Mbise (Leguruki), Emmanuel Salewa (Ngabobo), Joyce Ruto (Makiba) na Asanterabi Mbise (Maroroni). Ruto, Mollel na Mbise walidai wamejitoa kwa sababu ya kuzuiwa mawakala wao katika vituo vya kura kwa madai hawana utambulisho kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi.
Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Elias Mungure alisema katika kata hizo tano, taratibu nyingi za uchaguzi zimekiukwa na hivyo wameona hakuna sababu za kuendelea na uchaguzi huo. Alisema wagombea wote jana waliandika barua rasmi za kujitoa kushiriki uchaguzi huo. Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini, Pauline Gekul (Chadema) na wafuasi wanne walitiwa mbaroni Kata ya Leguruki wilayani Aremeru kwa tuhuma za kuzuia wananchi kwenda kupiga kura na kutafuta wananchi wenye umri mkubwa ili wawape kadi zao za kupigia kura.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alithibitisha kukamatwa kwa mbunge huyo na watu wengine wakizuia wananchi kupiga kura kwa madai hakuna mawakala wa vyama vyao vya siasa. Kata ya Murriet Arusha, baadhi ya changamoto zilikuwa mawakala kutotambua vituo vyao vya kupigia kura na wengine kukosa barua za utambulisho wa vyama vyao katika kata hiyo.
Msimamizi wa Uchaguzi Kata ya Murriet, Suleiman Kikinga alisema hakuna upungufu wa vifaa vya kupigia kura kwani vilipelekwa mapema asubuhi katika vituo 41 vya kata hiyo. Mkazi wa Kwa Mrombo, Elias Bichokora alisema uchaguzi ni mzuri na hali ya usalama ni nzuri ingawa mwitikio wa wananchi ulikuwa mdogo. Matokeo ya awali yalionesha CCM kuwa mbele katika kata hiyo.
Wakati Chadema ikijitoa, matokeo yameonesha katika kata hizo za Arumeru, CCM ilikuwa inaongoza katika vituo vingi ikiicha kwa mbali kabisa Chadema, hali inayoonesha kuwa itarejesha kata ambazo zilikuwa zimekwenda upinzani katika Uchaguzi Mkuu wa 2015. Mkoani Morogoro, katika Kata ya Kiroka katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro ulifanyika jana kwa njia ya amani na utulivu mkubwa.
Katika uchaguzi huo jana, wapigakura walioandikishwa ni 6,295 na kulikuwa na wagombea watatu, Jamila Mohamed kupitia CCM, Ngozoma Rahim wa Chadema pamoja na Jastah Mbena wa Chama cha Wananchi (CUF). Msimamizi wa Uchaguzi wa majimbo ya Morogoro Kusini na Morogoro Kusini Mashariki, Sudi Mpili alisema hadi saa 10 jioni, wananchi walikuwa wamepiga kura na kubakia kazi ya kuhesabu kura kwenye vituo na kutarajia kutangazwa kwa matokeo kabla ya saa mbili usiku.
Kata nyingine iliyofanya uchaguzi ni ya Sofi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi. Mkoani Dar es Salaam, baadhi ya wananchi waliopiga kura Kata ya Saranga, Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo, wamepongeza utaratibu uliotumika kutokana na kutokuwepo na foleni. Wananchi hao walisema wamezoea kwa kawaida katika vituo vya kupigia kura kukuta msongamano na foleni kubwa, lakini katika uchaguzi huo jana hapakuwa na foleni vituoni.
Gazeti hili lilipita katika baadhi ya vituo vya kupigia kura katika kata hiyo kujionea hali halisi. Akizungumza baada ya kupiga kura, mkazi wa Kimara Stopover, Margareth Nderumakialisema utaratibu ni mzuri na alipiga kura moja kwa moja bila kukaa foleni. Naye Chande Ligeni wa Kimara alisema ametumia haki yake ya msingi ya kumchagua kiongozi anayemtaka na kusema hapakuwa na usumbufu katika vituo vya kupigia kura.
Hata hivyo, baadhi ya vituo, Shule ya Msingi Mavurunza waandishi wa habari walizuiwa kutochukua taarifa wala kupiga picha kwa madai Mkurugenzi hajatoa kibali kwa waandishi. Akizungumzia uchaguzi huo kwa njia ya simu, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Kisare Makori alisema uchaguzi umefanyika vizuri na vituo vilifunguliwa asubuhi kuwapa wananchi fursa.
Alisema vituo vipo 129 na hali ya usalama imeimarishwa lakini taarifa zaidi kuhusu uchaguzi huo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ubungo ndiye anaweza kuzitoa kwa usahihi. Kata ya Kijichi Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam umefanyika kwa amani ingawa watu waliojitokeza kupiga kura ni wachache.
Gazeti hili lilitembelea vituo vya uchaguzi na kubaini changamoto hiyo huku wasimamizi wa uchaguzi na mawakala wakidai wananchi hawaelewi faida za kupiga kura na hawakushiriki mikutano ya kampeni ya wagombea. Vyama vilivyoweka wagombea wake katika kata hiyo ni Chama Cha Mapinduzi (CCM), ACT Wazalendo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), NCCR Mageuzi, Alliance for Democratic Change (ADC) na Chama cha Wananchi (CUF).
“Mwamko wa watu kupiga kura ni mdogo, watu waliojitokeza ni wachache na wanakuja kwa kusuasua hatuelewi tatizo ni nini wakati hali ni ya utulivu kabisa,” alisema msimamizi wa uchaguzi katika kituo cha Kijichi A kilichopo katika Shule ya Msingi Mtoni Kijichi. Alisema wananchi waliofika kupiga kura walipiga bila usumbufu wowote na hakukuwa na malalamiko yoyote kutoka kwa wananchi na pia mawakala wa vyama.
Vituo vya Mgeninani ofisi za Serikali ya Mtaa, wasimamizi wa uchaguzi na mawakala walisubiri wapiga kura. “Hali ya kituo ni shwari ingawa tunakaa hata nusu saa hajatokea mtu kuja kupiga kura, mfano kituo chetu kina majina 432 waliotakiwa kupiga kura lakini mpaka saa tisa hii waliopiga ni kama 100, alisema Epifania Tembo msimamizi wa kituo namba tano Mgeninani. Shaban Juma mkazi wa kata hiyo alidai watu waliopiga kura ni wachache kwa sababu uchaguzi huo unarudiwa mara ya tatu baada ya madiwani wawili kufariki nyakati tofauti.
CHANZO HABARI LEO

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa