Arusha
Home » » TAARIFA KWA UMMA JUU YA ZOEZI LA KUONDOA MIFUGO NA MAKAZI NDANI YA HIFADHI YA TAIFA SERENGETI NA KWENYE MPAKA WA PORI TENGEFU LOLIONDO

TAARIFA KWA UMMA JUU YA ZOEZI LA KUONDOA MIFUGO NA MAKAZI NDANI YA HIFADHI YA TAIFA SERENGETI NA KWENYE MPAKA WA PORI TENGEFU LOLIONDO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII

TAARIFA KWA UMMA

ZOEZI LA KUONDOA MIFUGO NA MAKAZI NDANI YA HIFADHI YA TAIFA SERENGETI NA KWENYE MPAKA WA PORI TENGEFU LOLIONDO

Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Ngorongoro, kwa kushirikisha Hifadhi ya Taifa Serengeti na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, inaendesha zoezi la kuondoa mifugo na makazi ndani ya hifadhi ya Taifa Serengeti na kwenye mpaka wa Pori Tengefu Loliondo.

Zoezi hilo lililoanza tarehe 10  Agosti 2017  litadumu kwa siku kumi na nne na linashirikisha Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Ngorongoro, Jeshi la Polisi, Usalama wa Taifa, Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Hifadhi ya Taifa Serengeti na Hifadhi ya eneo la Ngorongoro.

Zoezi hilo linalenga kunusuru uhifadhi ndani ya hifadhi, ndani ya Pori Tengefu Loliondo, na ndani ya mfumo ikolojia wa Serengeti na pia kunusuru utalii katika mfumo ikolojia huo.

Aidha, hatua hii ya kuondoa makazi na mifugo kutoka katika maeneo ya mipaka ya Pori Tengefu Loliondo kutaongeza uhakika wa kupatikana malisho ya mifugo wakati wa kiangazi kwa kuwa hakutakuwepo na makazi ndani ya Hifadhi na ufugaji holela.

kimsingi zoezi hili linaendana na wito wa Serikali wa kuondoa mifugo ndani ya maeneo yote yaliyohifadhiwa nchini.

Katika kutekeleza zoezi hili, Mkuu wa Wilaya  Ngorongoro, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Ngorongoro Bwana Rashidi Taka, alitoa maelekezo yafuatayo:

1. Zoezi litafanyika ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti na kwenye mpaka wa Pori Tengefu Loliondo. Kwa upande wa mpaka wa Pori Tengefu Loliondo zoezi litaanzia kaskazini hadi kusini urefu wa kilometa 90, na upana wake utakuwa kilometa 5. Kwa ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti litafanyika upande wa mashariki kuanzia milima ya Kuka (kaskazini) hadi kigingi na. SNP 9 (kusini); 

2. Maboma yatakayokutwa ndani ya hifadhi yatateketezwa kwa moto na watu watakaokutwa na mifugo watachukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kupelekwa mahakamani;

3.  Maboma yaliyoko ndani ya mpaka wa Pori Tengefu Loliondo -  kwenye mpaka na ndani ya kilometa tano - wataondolewa ili warudi vijijini. Eneo hilo litabaki kwa ajili ya malisho na si kwa ajili ya makazi.  Uwepo wa makazi kwenye mpaka wa Hifadhi ya Taifa Serengeti umekuwa kichocheo kikubwa cha mifugo kuingizwa hifadhini.

Zoezi hili linalenga kuondoa changamoto kubwa ya mifugo kuingizwa Hifadhi ya Taifa Serengeti na kwenye mpaka wa Pori Tengefu Loliondo, kupambana na uvamizi mkubwa uliofanywa na wahamiaji haramu kutoka nchi jirani na kunusuru vyanzo vya maji kutokana na mifugo kulishwa kwenye vyanzo vya maji na hivyo kusababisha vyanzo hivyo kuharibika na kukosekana kwa maji kwa ajili ya mifugo na wanyamapori.

Hadi sasa zoezi hili la kuondoa mifugo na makazi ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti na kwenye mpaka wa Pori Tengefu Loliondo linaendelea vizuri likihusisha kuchoma moto maboma yote yaliyoachwa na wafugaji walioondoka wakati wa zoezi.

Wizara ya Maliasili na Utalii inapenda kuufahamisha umma kuwa hakuna watu wanaopigwa katika zoezi hili.

Pia, Wizara ya Maliasili na Utalii inapenda kuutaarifu umma kuwa habari zinazosambazwa mitandaoni ni upotoshaji wa ukweli wenye nia ovu ya kujenga chuki dhidi ya Serikali  kwa wananchi wa Loliondo na maeneo yanayopitiwa na zoezi hilo.

Aidha, Wizara ya Maliasili na Utalii, inapenda kuweka bayana kuwa, taarifa za kupigwa risasi Pormoson Losso mwenye umri wa miaka 23, mkazi wa Ololosokwan zilitolewa tarehe 8 Agosti 2017 na hazihusiani na zoezi tajwa kwani tukio hilo  lilitokea siku tano kabla ya kuanza zoezi la kuondoa mifugo na makazi ndani ya hifadhi wakati zoezi hili lilianza kutekelezwa Jumapili tarehe 13 Agosti 2017.

Hata hivyo Serikali inawapongeza wananchi wengi miongoni mwa wafugaji kwa kuunga mkono zoezi hili na kwa ushirikiano wanaotoa.
Serikali inatoa onyo kwa yeyote anayejihusisha na upotoshaji wa ukweli kuhusu zoezi hili lenye nia njema linalolenga kunusuru hifadhi, kuacha mara moja ili kujiepusha na hatua za kisheria zitakazochukuliwa pindi atakapobainika.

Imetolewa na;

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

17/08/2017

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa