Arusha
Home » » CCM, Chadema watishia bastola Arumeru

CCM, Chadema watishia bastola Arumeru


Peter Saramba, Arusha
POLISI wilayani Arumeru inamshikilia Kada wa CCM, Edward Simon maarufu kama Bosco kwa tuhuma za kumtishia kwa bastola mfuasi wa Chadema.Kada huyo wa CCM, anatuhumiwa kutishia kumuua kwa kumpiga risasi mfuasi wa Chadema, Boniface Kimario aliyekuwa akipita mitaani kutangaza mkutano wa hadhara wa chama chake uliotarajiwa kufanyika eneo la Sasi.
Hatua ya kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo ilikuja baada ya aliyetishiwa kufungua jalada la malalamiko Kituo cha Polisi cha USA-River na kupewa namba ya mashtaka USR/RB/4245/2012, kosa la kutishia kuua kwa silaha.
Mtuhumiwa huyo aliyewekwa rumande baada ya kufikishwa kituoni hapo na polisi aliyekuwa akitumia usafri wa pikipiki.
Mratibu wa Kampeni za Chadema katika kata hiyo, Henry Kileo alisema wakati akitishiwa kuuawa kwa kupigwa risasi, Kimario alikuwa akitekeleza jukumu la kutangaza mkutano wao wa hadhara na baadaye kwenda kumfuata mgombea wa Chadema, Peter Msere nyumbani kwake Kijiji cha Bangata.
Kileo alisema wakati Kimario aliyekuwa kitumia gari aina ya Range Rover, ghafla mtuhumiwa alijitokeza na kuziba barabara kwa kutumia gari lake ndogo aina ya Rav 4 na kuchomoa bastola, kabla ya kutishia kumpasua kichwa kwa risasi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Lebaratus Sabas alisema hajapa taarifa hizo, kwa sababu bado suala hilo linashughulikiwa na polisi wilayani Arumeru na kuahidi kufuatilia.
Mkoa wa Arusha unafanya chaguzi ndogo katika kata mbili za Bangata, Arumeru na Daraja II mjini Arusha ikiwa ni kati ya kata 28 zinazofanya chaguzi ndogo, baada ya nafasi hizo za udiwani kubaki wazi kutokana na sababu mbalimbali.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Arusha Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa